Je unaweza kuwa Kiongozi?

Author: Malega Williams 1 year ago

Dhana ya uongozi ni pana na imejengeka katika jamii kwa mtazamo tofauti kulingana na mtu anavyochukulia. Uongozi upo katika siasa, makundi mbalimbali ya kijamii na upo katika biashara pia. Je kuna vitu vya tofauti vinavyomtofautisha kiongozi na watu wengine? Je kila mtu anafaa kuwa kiongozi? Au tufanyaje kutambua kiongozi bora? Haya ni aadhi ya maswali ambayo watu wengi hujiuliza linapokuja suala la kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi katika nyanja au mahali fulani. Katika nyanja ya siasa na harakati za kijamii tumeshuhudia viongozi wachache kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakikumbukwa na kuchukuliwa mifano ya uongozi wao hata baada ya kustaafu au kufariki dunia, ila wengine wanasahaulikwa mara tu wanapomaliza muda wao wa uongozi. Katika makala haya tutazungumzia sifa mbalimbali muhimu zinazomtofautisha kiongozi na watu wengine. Kwa kawaida lazima kuwe na pande mbili; kiongozi/viongozi na upande wa wale wanaoongozwa ambao katika makala hii nitawaita wasindikizaji au wafuasi. Mtu huwezi kujiita kiongozi au ukawania uongozi kama hujui unasimamia nini. Tabia ya kwanza kabisa ya kumpima kiongozi na kumtofautisha na wafuasi ni ile hali ya kuwa na maono (Vision) ya kipekee yanayomwongoza katika kusimamia mwelekeo fulani. Sio kila mtu anaweza kuwa na maono. Kiongozi kwa maana nyingine ni mbeba maono. Mtu mwenye maono anakuwa na uwezo wa kuona kitakachotokea siku za mbeleni. Kazi kubwa yakiongozi inakuwa ni kuwaelezea watu kuhusiana na maono yake na kuwashawishi ili waweze kuelewa na kukubaliana nae katika kufikia hatma anayoiona. Kama mtu hataweza kuwa na ushawishi wa hali ya juu kiasi cha kupata wafuasi wengi wanaomwamini katika maono uliyonayo basi mtu huyo atabaki kuwa tu mfuasi na si kiongozi. Kuwa na maono ni jambo la kwanza katika uongozi, ila kuweza kubadilisha maono/ndoto kwenda kwenye matendo na uhalisia ni jambo la pili. Katika hili ndipo kwenye kazi kubwa sana. Kuna kazi kubwa kwa sababu huwezi kufanya yote yatokee ukiwa mwenyewe bila kuwa na watu wenye mtazamo kama wako na wenye kuelewa kinagaubaga juu ya maono uliyonayo na mwelekeo unaotaka kwenda. Uwezo wa kiongozi kujenga timu imara yenye uelewa na morali ya kutosha juu ya wanachopaswa kufikia ni karama ya pekee ambayo inamtofautisha kiongozi na watu wengine. Ili kuwa na timu imara na iliyo bora, kwanza kiongozi lazima aweze kutambua tabia na uwezo wa kila mmoja kati ya watu alionao. Hii itamsaidia kujua nani atapewa majukumu gani na kuyafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa. Watu ndio hazina kubwa ya kumwezesha kiongozi yeyote kufikia malengo makubwa aliyojiwekea. Kwa kawaida kiongozi mzuri anaweza kuwatambua na kufanya kazi na watu wenye upeo mkubwa na wanaoweza kusaidia katika kufanikisha azma iliyowekwa. Viongozi walioweka historia katika hili ni pamoja na Alexander the Great, Mwl. JK Nyerere baba wa Taifa wa Tanzania, Mao ambaye ni Rais wa kwanza wa China, Rais wa kwanza mweusi Afirka ya Kusini Nelson Mandela, Bill Gate mwanzilishi wa kampuni kubwa ya Microsoft, Ford, Steve Jobs na wengineo. Kuwa na ushawishi wa hali ya juu ni jambo la msingi katika suala zima la uongozi. Ushawishi ni uwezo wa kuwafanya watu wengine waweze kuamini, kufikiria na kutenda yote wanayoambiwa au wanayopata kutoka kwako. Ili uweze kujenga ushawishi ni lazima uwe umekuwa na mahusiano mazuri baina yako na wale unaowaogoza. Bila kuwa na mahusiano mazuri hakuna kinachoweza kufanyika kwani unaowaongoza watakuwa wanaona kama unawaonea au unawaongoza bila waokukupenda. Kiongozi mwenye mahusiano mazuri na wale anaowaongoza lazima atakuwa kati yao, atakuwa mfuatiliaji na msikilizaji mzuri na kujua kila kitu ambacho kinafanyika. Atatoa mwongozo na kuhakikisha unatekelezwa huku yeye akiwa kama mfano katika utendaji.Kwa kufanya hivyo, wafuasi wake watakuwa wanampenda na kutaka awe kiongozi wao daima na kupenda kufuata nyayo zake bila ya kushurutishwa. Hii ndio sifa pekee inayomtofautisha kiongozi mzuri na bosi. Wakati bosi akikaa nyuma na kuelekeza, kiongozi anakaa na watu wake na kuwaelekeza nini cha kufanya huku wakifanya kwa pamoja. Mara nyingi ufanisi mkubwa wa kiongozi huonekana baada ya yeye kuachia nafasi ya uongozi aliyokuwa nayo au kufariki dunia. Kama alikuwa kiongozi mzuri, atabaki akikumbukwa daima kwa miaka nenda rudi juu ya yale mazuri aliyokuwa anayapigania, yale aliyofanikiwa kuyafanya na falsafa zake wakati akiwa kiongozi hazitakufa nae bali zitaendelea kuishi kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hii tunaiita uwezo wa kuacha urithi (legacy) katika fikra za wale wanaoendelea kuishi. Kama kiongozi alikuwa na maono mazuri juu ya jamii yake na akaishi vizuri na watu huku akiwaongoza kwa mifano , basi kiongozi huyu hawezi kufa na kusahaulika. Tunaweza kuchukua mifano ya viongozi kama waliotajwa hapo awali pia tukaongezea Martin Luther King kiongozi aliyepigania haki ya jamii ya watu weusi kule Marekani kipindi chote cha uhai wake. Maono na falsafa zake zimedumu hadi leo zinaongelewa duniani kote. Kufikia hapa tumeweza kuona baadhi ya vitu vya tofauti kati ya makundi haya mawili; viongozi na wafuasi /wasindikizaji. Kuna watu wengi wangependa kuwa viongozi katika nyanja mbalimbali zikiwemo siasa, jamii, kampuni n.k. hawana budi kuelewa utofauti uliopo na kuanza kujitathimini. Katika makala ijayo tutazama ndani kabisa na kuchimbua mambo muhimu ya kufanya katika kuwa na maono na jinsi ya kujenga ushawishi ili uweze kuwasilisha maono uliyonayo katika hali ya kueleweka na kukubalika na wafuasi unaowataka.